Uwaridi Official

Ukurasa maalumu wa Umoja wa Waandishi wa Riwaya wenye Dira (UWARIDI)

Photos from Uwaridi Official's post 28/07/2024

HONGERA TENA, Laura Pettie , KWA TUZO NYINGINE...

Julai 27, 2024 - JANA - MwanaUWARIDI Laura Pettie, alipokea Tuzo ya kimataifa ya iChange Nations International Awards, pale JNICC.

Tuzo hii imemtambua Laura wetu k**a Mwandishi wa Riwaya mwenye...
- Maandishi yanayoleta mwangaza.
- Kalamu inayoleta mabadiliko chanya.
- Matendo yanayorudisha matumaini kwa jamii.

UWARIDI tunajivunia sana hatua hii na tunampongeza Laura, k**a jinsi nanyi mnavyompongeza hivi sasa, kwa kutunukiwa tuzo hii kubwa.

Kila la heri Laura!

07/07/2024

Takribani watu milioni mia mbili Duniani tunazungumza Kiswahili—na kukifanya kuwa lugha ya nane kati ya lugha elfu sita zinazo zungumzwa. Ni fahari kubwa kwetu kuzungumza, kusoma na kuandika kwa Kiswahili.

Kiswahili: Elimu na Utamaduni wa Amani.

Ikulu Mawasiliano Msemaji Mkuu wa Serikali

26/06/2024

Bingwa wa taharuki HUSSEIN TUWA ametuletea kitabu cha MUUAJI WA MWAKA MPYA, kinachokujumuisha hadithi fupi fupi, zikiongozwa na riwaya ya “Muuaji wa Mwaka Mpya” yenyewe.
K**a u-mpenzi wa riwaya kwa ujumla, basi hupaswi kukikosa kitabu hiki, na k**a wewe ni mpenzi wa hadithi fupi fupi, basi hakika hiki ni kwa ajili yako.
Kitabu kinauzwa shilingi za kitanzania ELFU KUMI NA TANO TU (15,000/-); na kinapatikana kwenye maeneo yafuatayo:

DAR ES SALAAM:

1) Duka la Kona ya Riwaya - Kinondoni Block 41 (0655 428085)

2) Posta Mpya - Kwa George (0755 454152)

3) Elite Bookstore - Tangi Bovu

4) Duka la Kalamu Tulivu (Kwa Molito) - Magomeni Kanisani, mtaa wa Limbeni - (0718 975659)

NJE YA DAR ES SALAAM:

ARUSHA — Chuo cha Makumira: Kwa Mariam (0683 703 275)

MBEYA – Kwa Edna Tibandelana (0754 0910481)

MOROGORO – Kwa Markus Mpangala (0719 226 293)

Kwa mikoa mingine tutaweza kumfikishia msomaji mpaka alipo, kwa kuwasiliana moja kwa moja na duka letu la KONA YA RIWAYA kwa namba iliyotajwa hapo juu (0655 428085).

13/05/2024

WAANDAAJI TUZO YA MWALIMU NYERERE 'WALIVYOKURUPUKA' DHIDI YA USHINDI WANGU WA 2023

NIANZE kwa kurudia tena kuipongeza Serikali yetu kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuanzisha Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu.

Ninasema ninarudia kupongeza kwa sababu Aprili 17, 2024, ikiwa ni siku chache baada ya awamu ya pili ya tuzo hizi kutolewa, niliandika andiko la kupongeza sambamba na kutoa hoja kadhaa nikilenga wahusika kuboresha hapa na pale katika mashindano yajayo wakiona inafaa.

Pamoja na mimi kutangazwa mshindi wa kwanza wa tuzo hiyo katika kipengele cha riwaya, nilitaraji ushauri wangu ungefanyiwa kazi katika kuboresha tuzo hizi. Lakini mambo yanayotokea, hususani baada ya mashindano ya mwaka huu yananiachia maswali mengi kuhusu mustakabali wa mashindano hayo na hofu yangu ukiwa usahihi wa baadhi ya hatua zinazochukuliwa na chombo kilichokabidhiwa jukumu la kuendesha tuzo hizi, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET).

Ni kwamba, wiki iliyopita, TET waliniandikia barua yenye nia ya kutengua ushindi wa wangu wa tuzo hizo upande wa riwaya nilioupata mwaka jana, wakidai wamefanya uchunguzi na kugundua kwamba muswada huo ulishawahi kuchapawa mtandaoni.

Kilichonishangaza ni sababu za kutengua walizosema. Kadri ya barua yao walioniandikia ni kwamba wametumia vigezo vya tuzo za mwaka huu wa 2024 kutengua ushindi wangu wa mwaka 2023 k**a nitakavyofafanua!

Vigezo vya tuzo za mwaka jana vilikuwa ni pamoja na “Muswada usiwe umechapishwa na mchapishaji au kuchapishwa binafsi.” Kimsingi, neno mchapishaji humaanisha kampuni za kuchapa vitabu (traditional publishing houses) na kuchapishwa binafsi (self publishing) humaanisha hatua ya mtunzi binafsi kufanya uhariri, kuandaa jarida, kuandaa masoko na kuchapa kitabu kwa raslimali zake. Kwa kifupi kigezo hicho kinahusu kitabu. Nimejaribu kutafuta maana ya 'kuchapisha binafsi' kunakonihusu mimi zaidi hadi kutumia Akili Mnemba, nikapata jibu la ufahamu uleule niliokuwa nao mwaka jana.

Mwaka jana wakati ninapeleka muswada wangu kushindania tuzo hizo, nilijua kwamba sehemu tu ya mswada ule iliwahi kubandikwa mtandaoni, lakini vigezo havikuwa vinanizuia kwa kuwa muswada ulikuwa haujawahi kuchapishwa kitabu.

Katika mashindano ya kupata washindi kwa ajili ya tuzo za mwaka huu, vigezo vilikuwa ni pamoja ha hivi: “Sehemu yoyote ya miswada isiwe imechapishwa na mchapaji au kuchapishwa binafsi pamoja na kuchapishwa mtandaoni.”

Katika barua ya TET kwangu ya Mei 9, 2024, kwanza wamesema wanatengua ushindi wangu kwa kuwa muswada wangu ‘umechapwa mtandaoni” na kunitaka nirudishe tuzo zote nilizopata mwaka jana ikiwa ni pamoja na fedha. Nimeshawaandikia barua ya kupinga.

Tena barua yao haikuwa inanieleza kukusudia kuutengua bali inaonesha wamekwishaamua. Kwa lugha nyingine, barua yao haikuzingatia kile wanasheria wanaita haki ya kusikilizwa kwanza (principle of natural justice).

Nimewajibu kwa sababu ya uungwana tu kwani ningeweza kukaa kimya kwa kutopewa haki yangu k**a mwanadamu ya kusikilizwa (condemned unheard).

Nimekuwa pia ninajiuliza imekuwaje TET katika hili wanakwenda kinyume na Sheria ya Mapokeo (Common Law Principle) kwani kwa mujibu wa mwanasheria wangu, unapotaja kitu kimoja na kuacha kingine ina maana kile ambacho hakikutajwa hakihusiki (mention of one thing is exclusion of another).

Maana yake ni kwamba k**a waandaaji walidhamiria muswada usiwe pia umechapishwa kwenye mtandao wangeweka hicho kigezo k**a walivyoweka mwaka huu.

Swali lingine la kujiuliza ni kwamba k**a TET wanadhani katika vigezo vya mwaka 2023 pia vilihusu muswada kutochapishwa kwenye mtandao na kwamba washiriki wangeelewa dhamira hiyo bila kukitaja kigezo hicho, kwa nini katika shindano la 2024 wametaja kigezo cha kuchapisha mtandaoni bayana?

Lakini uchunguzi wangu kwenye mitandao pia unaonesha kwamba hatua hii ya TET kutaka kutengua ushindi wangu halali pengine imetokana na andiko la mshiriki mwenzangu wa mwaka jana akilalamika kwamba nilikiuka vigezo. Ingawa kwa sasa ameliondoa andiko lake mtandaoni lakini watu walishalinakili (sharing).

Ninachoweza kusema, wote waliomuunga mkono bwana huyo 'waliingia mkenge' kwa sababu hakuweka wazi kwamba vigezo vya mwaka huu na mwaka jana ni tofauti. Kinachonishangaza ni kwa TET pia kusahau kwamba vigezo vya mwaka huu ni tofauti na vya mwaka jana.

Kwa bahati nzuri (au mbaya kwa wengine), mshindi wa kwanza wa mwaka huu, Laura Pettie na mimi mshindi wa mwaka jana, wote ni wanachama wa Umoja wa Waandishi wa Riwaya wenye Dira (UWARIDI). Wasichokijua watu ni kwamba miswada yetu inapitiwa na wahariri makini.

Lakini ni ukweli pia kwamba kuna watu wanatumia mitandao kutaka kuharibu taswira nzuri ya UWARIDI ambayo imekuwa ikitoa waandishi bora na hata washindi kwenye tuzo mbali mbali. Wanaokerwa na UWARIDI, walijaribu pia kuchokonoa ushindi wa mwaka huu kwa kumpaka matope mshindi wa kwanza katika kipengele cha riwaya bila mafanikio.

Ninawashauri pia TET wasifanyie kazi makelele ya mitandaoni ( hizi ni hisia zangu tu). Vinginevyo inaleta hofu kwa watu makini kushiriki tuzo ambazo kelele zinafanyiwa kazi badala ya weledi na hivyo mshindi hawezi kukaa akijiamini kwamba hilo limepita.

Kutokana na uzito wa jambo hili, endapo barua yangu haitojibiwa na/au wakaendelea kubaki na msimamo huo, nitalifikisha suala hili mahak**ani ili kupatiwa haki yangu.

Pamoja na makala hii, ninaambatanisha vigezo vya tuzo ya mwaka jana na ya mwaka huu, pamoja na maana ya Mchapishaji Binafsi kwa mujibu wa AI.

29/04/2024

Safari hii kwenye "Swahili Story" ya TWIGA INFLIGHT Magazine ndani ya ndege za Air Tanzania, kalamu ya mwandishi mahiri kutoka Uwaridi, Sharifa Nyanga ( Sheri Counsellor ), inaipaisha angani lugha adhimu ya Kiswahili kwa hadithi fupi "Msiba wa Kujitakia".

18/04/2024

UWARIDI NA TUZO

Salaam!

Tangu kutangazwa kwa washindi wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu kwa mwaka 2024, kumekuwa na minong'ono huko mtandaoni juu ya mambo kadha wa kadha kuhusu washindi wa tuzo, majaji wa tuzo, nk. Isivyo bahati, si jukumu la UWARIDI kuwasemea waandaaji. Lakini, kwakuwa kuna maeneo ambayo UWARIDI tumetajwa moja kwa moja, hatuna budi kutoa ufafanuzi katika maeneo hayo tu ili kuepusha upotoshaji dhidi yetu.

MWANACHAMA WA UWARIDI KUWA JAJI.
Mmoja kati ya wanachama wa Uwaridi, ndugu Fadhy Mtanga, aliteuliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kuwa miongoni mwa MAJAJI TISA wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu kwa mwaka 2024, k**a ilivyowekwa wazi na Mwenyekiti wa K**ati ya Tuzo, Prof. Penina Mlama, kwenye siku ile ile ya hafla ya utoaji wa tuzo. Malalamiko ya baadhi ya waandishi ni kwamba, Mshindi wa Tuzo hiyo katika nyanja ya riwaya, Bi Laura Pettie, ni mwanachama wa Uwaridi. Hivyo, wanadhani huenda Fadhy alifanya upendeleo kwa Laura.

Kwanza kabisa, hakuna Mwanachama wa Uwaridi aliyekuwa anafahamu kuwa Fadhy Mtanga ameteuliwa kuwa jaji mpaka ilipotangazwa rasmi siku ile ile ya utoaji wa tuzo, muda ambao majaji walikuwa wamekwishamaliza kazi yao. Hiyo ilikuwa ni moja kati ya masharti ya kuwa jaji: Usiri. Hivyo si Laura, wala mwandishi mwingine yeyote wa UWARIDI aliyekuwa akijua kwamba Fadhy ameteuliwa kuwa jaji. Na hili limekuwa hivyo kwa kuwa Fadhy alikuwa na ukomavu stahiki wa kutunza siri aliyoapishwa kuitunza, na waandaaji wa Tuzo.

Pili, kwa mujibu wa ufafanuzi wa Mwenyekiti wa K**ati ya Tuzo ni kwamba, K**ati inapopokea miswada ya waandishi, kwanza huichambua na kisha ile iliyokidhi vigezo hupelekwa kwa majaji ikiwa imekwishaondolewa majina ya waandishi husika na kuwekewa alama maalumu. Hivyo, si tu Fadhy pekee, bali hapakuwa na jaji mwingine yeyote aliyekuwa anajua mswada flani ni wa mwandishi flani. Utaratibu huu umewekwa na waandaaji wa tuzo ili kudhibiti usiri wa washiriki wakati wa mchakato.

Tatu, si kila jaji alihusika kusoma na kuhukumu kila mswada katika kila nyanja. Mfano, mwaka huu majaji walikuwa TISA tu: watatu kwenye riwaya, watatu kwenye ushairi na watatu kwenye hadithi za watoto. Fadhy hakuteuliwa kuwa jaji kwenye nyanja ya RIWAYA. Hivyo, si tu haku-jaji mswada wa Laura, bali pia hakusoma mswada wowote wa riwaya kutoka kwa mwandishi yeyote.

Nne, mtu yeyote atakayeteuliwa kuwa jaji ni lazima awe ni mtaalamu, mjuzi na mdau katika tasnia ya uandishi bunifu. Fadhy ni mtaalamu na mshirika mahiri katika fasihi nchini mwetu. Anaaminika si tu na waandaaji wa tuzo k**a hii ya Mwalimu Nyerere bali pia taasisi nyinginezo za ndani na nje ya nchi. Mfano rahisi ni Shirika kubwa kabisa la Uchapishaji nchini Marekani liliamua kuingia gharama kubwa kumsafirisha hadi San Francisco kwa ajili ya shughuli za kifasihi, baada ya kuuona uwezo wake wa kiuandishi na kuutambua weledi wake, kupitia kazi na machapisho yake mbali mbali.

Kwa hivyo, Tuzo ya Mwalimu Nyerere hawakukosea kumchagua Fadhy kuwa miongoni mwa majaji. Jaji hawezi kutoka Bongo Movie, Bongo Fleva au Shirikisho la Soka, bali atatokana na waandishi wenyewe ima UWARIDI, Ukuta, Bakita, Wakita, Uwavita, Tataki, nk. Mfano, mmoja kati ya majaji TISA wa mwaka huu 2024, ni Mwl. Richard Mabala, ambaye ni mwanachama wa Uwavita—na waandishi kutoka Uwavita hushiriki pia tuzo hizo. Lakini sijaona k**a kuna mlalamikaji yeyote aliyelalamikia mwanachama wa Uwavita kuwa jaji wa tuzo hizi. Je, jaji kutoka Uwavita (Mabala) angeweza kumruhusu jaji kutoka Uwaridi (Fadhy) kumpendelea mwandishi wa Uwaridi na ilhali yeye pia ana waandishi wenziye kutoka Uwavita? Sidhani k**a inahitaji rocket science kugundua propaganda hizi zenye nia ovu kwa Uwaridi.

Tano, bila kujali wanakotokea, Fadhy Mtanga na Mwl. Richard Mabala, wote wawili ni waandishi mahiri wa mashairi, riwaya, hadithi fupi fupi, makala, nk., ambao nchi yetu imebahatika kuwa nao. Hivyo wanastahili kutoa mchango wao katika tasnia hii kwa nafasi za u-jaji wa tuzo hizi.

UWEZO WA WAANDISHI WA UWARIDI
Umoja wa Waandishi wa Riwaya wenye Dira (UWARIDI) unajivunia uwezo wa waandishi wake na utaendelea kuwanoa kila uchao ili kuzifanya kazi zao kuwa bora na kutambulika zaidi. UWARIDI haina nia wala sababu ya kufanya hila ili kupata fursa flani (tuzo, nk), bali tutaacha kazi zetu zijitetee zenyewe k**a ambavyo zimekuwa zikifanya:

1. Mshindi wa Kwanza wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu kwa mwaka 2023, alikuwa ni bwana Hamisi Kibari. Huyu pia ni mwanachama wa UWARIDI. Lakini msimu huo, si tu hapakuwa na jaji kutoka UWARIDI, bali mmoja kati ya majaji wa mwaka huo 2023, bwana Majid Mswahili, ni mwanachama wa Uwavita. Je, hapo mwandishi wetu bwana Kibari alipendelewa na nani?

2. Mshindi wa Kwanza wa Tuzo ya Safal-cornell katika nyanja ya ushairi kwa mwaka ni 2023, alikuwa ni ndugu Salum Makamba. Huyu pia ni mwanachama wa UWARIDI —na msimu huo hapakuwa na jaji kutoka UWARIDI. Je, huyu naye alipendelewa na nani huko Kenya?

3. Mshindi wa SITA wa Tuzo ya Mwalimu Nyerere katika nyanja ya riwaya kwa mwaka 2023, alikuwa bwana David Shaba Shalali. Huyu naye ni mwanachama wa UWARIDI —na mwaka huo hapakuwa na jaji kutoka UWARIDI, je, alipendelewa na nani?

4. Mshindi wa PILI wa tuzo ya Hekaya Initiative ya nchini Kenya (Inayodhaminiwa na Mozilla), kwa mwaka 2023, alikuwa ni Bi Lilian Mbaga. Huyu naye ni mwandishi kutoka UWARIDI —na katika tuzo hizo hapakuwa na jaji kutoka UWARIDI. Je, huyu naye alipendelewa na nani huko Kenya?

5. Rais wa Umoja wa Waandishi wa Riwaya wenye Dira (UWARIDI), bwana Hussein Tuwa, naye pia ni mshindi wa Tuzo ya Macmillan na mshindi wa pili wa tuzo ya Burt Award for African literature. Je, naye alipendelewa na nani?

6. Mshindi wa TANO na mshindi wa TISA wa tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere kwa mwaka 2024, katika nyanja ya riwaya, bwana Kibari na bwana Shalali ni wanachama wa UWARIDI. Hawa nao walipendelewa?

Uwezo wa Laura Pettie kiuandishi, k**a ilivyo kwa waandishi wengine wa UWARIDI, unajieleza. Waliosoma kazi zake wanalifahamu hilo. Kamwe hahitaji kubebwa wala kupendelewa na mtu yeyote. Jamii ya wasomaji nchini inatambua umahiri wa Laura pamoja na wa waandishi wengine wa Uwaridi. Hata shangwe na nderemo kutoka kwa wasomaji nchi nzima vilivyorindima baada ya kutangazwa kwake kuwa Mshindi wa Kwanza wa Tuzo hii ya Mwalimu Nyerere, ni udhihirisho bayana wa namna anavyokubalika. Ni kioja cha mwaka k**a kuna mtu anaamini Laura anapendelewa.

Hoja pekee inayobakia kushadidiwa ni kwa nini Fadhy alifuta andiko lake Facebook kuhusu yeye kuwa jaji wa Tuzo muda mfupi baada ya mshindi (Laura) kutangazwa. Mtu yeyote makini akishaona yote yaliyoelezwa hapo juu, itamfunukia wazi kuwa hata hoja hii nayo haina uzito wa kimantiki.

K**a Uongozi tulimuuliza Fadhy kuhusu kadhia hiyo. Akatufafanulia vizuri kwamba, alikusudia ku-post andiko lile katika mitandao ya Twitter na Instagram pekee—na alifanya hivyo. Lakini alisahau kubadilisha settings za kwenye ukurasa wake wa Instagram, hivyo andiko lile likaji-post automatically kutoka Instagram mpaka Facebook [mtumiaji yeyote wa mtandao anaweza kulifahamu hili]. Alipogundua hivyo na kuamua kulifuta Facebook likafutika mpaka Instagram. Lakini hakufuta huko Twitter (ambako yuko active zaidi) kwakuwa ukurasa wake wa Twitter hauingiliani na kurasa zake nyinginezo. K**a angelikuwa na nia ovu basi angelifuta kila mahali, lakini mpaka sasa andiko lake liko katika ukurasa wake wa twitter.
Hili lilikuwa ni jambo dogo mno kwa mtu mtafiti na makinifu.

Mwisho kabisa, tunatoa wito kwa wadau wote wa fasihi kutumia fursa walizonazo kukosoa na/au kushauri jambo lolote lenye maslahi katika tasnia hii, kwa kuongozwa na nia njema pamoja na hoja za msingi, badala ya kulazimisha hoja za uongo na zenye kila dalili ya chuki dhidi ya taasisi fulani na/au kujitafutia umaarufu usio na maana.

UWARIDI, Njoo tunukie.

Photos from Uwaridi Official's post 16/04/2024

Pamoja na kumsherehekea mwanachama wetu wa Uwaridi Official, Bi Laura Pettie kuwa MSHINDI WA KWANZA wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, katika nyanja ya riwaya kwa mwaka 2024, tunatumia nafasi hii pia kuwapongeza wanachama wetu wengine: Bw. Hamisi Kibari kwa kuwa MSHINDI WA TANO na Bw. David Shalali kuwa MSHINDI WA TISA katika tuzo hiyo hiyo.

14/04/2024

MSHINDI WA KWANZA wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu katika riwaya, kwa mwaka 2024, ni mwanachama wa Umoja wa Waandishi wa Riwaya wenye Dira (Uwaridi), Bi Laura Pettie.

Hii ni mara ya pili kwa tuzo hii kuja UWARIDI. Mwaka 2023 mwanachama wetu mwingine, Bwana Hamis Kibari, alikuwa MSHINDI WA KWANZA wa riwaya katika tuzo hii.

Hongera sana Laura. Hongera Uwaridi.

08/03/2024

Kutoka kwetu, kuja kwenu... nyoooote!

06/03/2024

Rais wa UWARIDI Hussein Tuwa akiuongelea uzinduzi wa vitabu viwili vya Wilbard Makene... Machi 9, Saa 9 alasiri... pale Elite Bookstore Tangibovu.

Send a message to learn more

01/03/2024

Umoja wa Waandishi wa Riwaya wenye Dira (Uwaridi), tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunatoa pole kwa Watanzania wote.

28/02/2024

Mbiu Press inapenda kukukaribisha katika uzinduzi wa vitabu *(UCHOCHORO WA TANZANITE na UFAFANUZI LUGALO)* vilivyoandikwa na Mwandishi *Wilbard Makene*.

📍 𝐄𝐥𝐢𝐭𝐞 𝐁𝐨𝐨𝐤𝐬𝐭𝐨𝐫𝐞 𝐌𝐛𝐞𝐳𝐢 𝐁𝐞𝐚𝐜𝐡
📅 𝐉𝐮𝐦𝐚𝐦𝐨𝐬𝐢 𝐌𝐚𝐜𝐡𝐢 𝟗, 𝟐𝟎𝟐𝟒
⏰𝟎𝟗:𝟑𝟎 A𝐥𝐚𝐬𝐢𝐫𝐢 - 𝟏𝟐:𝟎𝟎 𝐉𝐢𝐨𝐧𝐢

*NB: Jisajili Mtandaoni upate nafasi ya kununua Kitabu chochote cha mwandishi Wilbard Makene kwa punguzo la 𝐀𝐬𝐢𝐥𝐢𝐦𝐢𝐚 𝟏𝟎*

*Kujisajili:* 🔗
https://forms.gle/2UxGWaJFXYYGiwBk9

𝐊𝐚𝐫𝐢𝐛𝐮𝐧𝐢 𝐍𝐲𝐨𝐭𝐞

01/01/2024
17/12/2023

𝐒𝐚𝐟𝐚𝐫𝐢 𝐲𝐚 𝐒𝐚𝐧 𝐅𝐫𝐚𝐧𝐜𝐢𝐬𝐜𝐨

MWAKA 1999 nilikuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu wa Shule ya Sekondari Njombe. Miongoni mwa vitu nilivyokuwa navyo, ni daftari kadhaa za nyimbo za reggae, R&B na Hip Hop. Kwenye moja ya daftari hizo, mimi na rafiki zangu tuliweka taarifa tulizoziita autobiography. Kwenye ukurasa wangu, sehemu ya Best City niliandika majiji mawili: Kingston, Jamaica (kwa sababu ya kupenda muziki wa Bob Marley), na jiji jingine, San Francisco, Marekani (nilikuwa nimeona filamu na picha kadhaa vikionesha daraja kubwa sana).

Nikimbize mkanda.

Sasa ni miaka 24 tangu nilipoandika vile.

Na leo hii, ninaandika hapa nikiwa orofa ya 5 ya hoteli ya Kimpton Alton, jijini San Francisco ndani ya jimbo la California hapa Marekani. Na wakati huu ikikaribia saa nne unusu ya asubuhi, ninafahamu ni saa tatu unusu nyumbani Tanzania. Kabla hujalala, nimeona nikuandikie kidogo. Na, nitaandika harakaharaka kwa kuwa ifikapo saa 5 nitaanza safari ya kupita kwenye handaki la chini ya bahari ya Pasifiki ili kuzuru jiji la Auckland.

Wakati nikikuandikia, tayari nimeshapita juu na chini ya Golden Gate Bridge kwa kutumia basi na boti mtawalia. Tayari nimeshapanda ngazi 234 kwenye orofa 13 za Mnara wa Coit. Nimeshatembelea Gereza la Alcatraz, gereza maarufu mno k**a ‘Mwamba’, tayari nimekwishatembelea mitaa yote ya San Francisco kwa basi maalumu. Nimekwisha panda milima na kushuka mitaa yote adhimu. Nimekwishakula chakula cha Kimeksiko, tacos; ya samaki, ya ng’ombe na ya kuku. Nimekwishakunywa miongoni mwa cappuccino bora zaidi ulimwenguni. Nimekwishazuru majengo marefu na ya kihistoria k**a kiwanda cha chokoleti cha Ghirardelli. Na zaidi, nimetembelea duka kubwa na kongwe la vitabu na uchapishaji la City Light.

Nisikuchoshe, kwa kuwa, kila kitu nitahitaji kukiandikia simulizi yake iliyosheheni. Na kwa kuwa naandika harakaharaka hapa, niseme kwa nini nipo San Francisco.

Mwezi Novemba 2021 niliandika hadithi fupi: Haiba. Na nikikusimulia kilichonisukuma kuandika, utacheka. Waswahili husema, heri huzaliwa katika tumbo la shari. Hii simulizi tuachane nayo.

Siku chache baada ya kuposti simulizi hiyo mtandaoni, mtu mmoja aliniandikia kupitia kibobo cha Twitter (nasikia siku hizi mnaita X) kuomba idhini yangu kuitafsiri kwenda Kiingereza. Sikuona shida. Nilimruhusu.

Mwezi mmoja baadaye, nikaandikiwa barua-pepe ya kuombwa akaunti yangu ili kulipwa kutokana na simulizi hiyo. Na kwa kuwa wakati huo nilikuwa njiani kuelekea mapumziko ya Krismasi na Mwaka Mpya, nikasema, ‘aaah, mambo si ndo haya!’

Miezi michache baadaye, nikaombwa idhini ya simulizi hiyo kutumika kwenye mkusanyiko wao wa kwanza wa simulizi kutoka Afrika Mashariki. Kwa hakika, nilikubali nikiwa na furaha tele. Kwangu, ilikuwa hatua adhimu mno katika uandishi wangu. Na wakati haya yakitokea, nilikuwa nimekwishafikiria kustaafu kuandika kutokana na sababu kadha wa kadha (hii ni simulizi ya wakati mwingine).

Nipeleke mbele zaidi simulizi.

Siku moja mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu, nilipokea barua pepe kwenye akaunti binafsi. Kwa kuwa kichwa kilianza na ‘Invitation to…’ nilitaka kuipuuza nikiamini ni zile barua pepe za kawaida zinazokuja mara nyingi. Kitu kikaniambia niifungue. Na nilipoona ni mwaliko wa kuja Marekani kuhudhuria maadhimisho ya miaka 10 ya kampuni m***i ya uchapishaji wa vitabu hapa Marekani, nikasema, ‘eeh b’ana eeh!”

Nilipojibu kukubali, nikapokea maelekezo yote na taratibu za kuomba viza zikafanyika kwa mafanikio. Na barua ya mwaliko ikanitaka kuja kusoma simulizi ya Haiba (ambayo inafahamika k**a Attitudes kwenye kitabu cha mkusanyiko wa riwaya kutoka Afrika Mashariki, No Edges). Na jambo la kuvutia, mfasiri wangu, Jay Boss Rubin alialikwa pia.Naye, alisoma tafsiri ya Kiingereza.

Nimesema naandika harakaharaka niwahi misele, si eti eeh? Najua nawe unataka kulala baada ya pilika za kutwa nzima.

Jana, kumefanyika maadhimisho hayo hapa San Francisco. Na kwa heshima kubwa, nilipewa nafasi ya kusoma kipande cha simulizi hiyo mbele ya wachapishaji na waandishi wakubwa. Fikiria, unasoma simulizi mbele ya mwandishi bingwa wa Kimeksiko, Jazmina Barrera, ama mfasiri nguli wa Kichina, Jeremy Tiang, ama mbele ya mhariri bingwa Kesley McFaul. Na baada ya kusoma, kwenye hafla ya usiku, nikaimba wimbo maarufu zaidi wa Kiswahili, Malaika.

Simulizi ni nyingi mno. Ninahitaji kuandikia kitabu chake mahsusi.

Wakati nataka kumalizia kwa leo, niseme hivi: Ushirikiano wangu na kampuni hii, ambayo pia imefanya kazi na mwandishi mwenzangu Lilian Mbaga (na mfasiri wake Dkt. Uta Reusterd) kwenye mkusanyiko huo wa No Edges, ni jambo kuntu mno. Ninaamini, safari yangu hii ya kuja kuwatembelea hapa Marekani inafungua njia muhimu kwa simulizi za Kitanzania. Ninaamini, safari hii inachonga barabara itumiwe na waandishi wenzangu wengi. Tanzania ina utajiri wa fasihi ya Kiswahili. Ambayo, k**a nilivyowaambia watu kwenye hafla ya jana, ni wa kipekee mno ukisawiri mambo kedekede kwenye nyanja zote za maisha.

Kuna raha sana kuzuru jiji kubwa la San Francisco. Ila raha zaidi, kupata wasaa wa kukuandikia haya.

Hadi wakati mwingine.

Fadhy Mtanga,
Kimpton Alton Hotel,
2700 Jones Street,
San Francisco, California.

15 Desemba 2023.

07/10/2023

Twasemaje....?
Ni sisi ndiyo tunaoendelea kukiweka kiswahili angani na duniani! Ni kupitia Twiga Inflight Magazine ya Air Tanzania! Safari hii ni mwamba wa masimulizi ya malavidavi, Fadhy Mtanga - ambaye ametulea habari za "Marafiki Wawili."
Msome angani!

UWARIDIIII!

19/09/2023

Tunaendelea kukiweka Kiswahili ANGANI!
Safari hii tumepaa na bingwa wa ushairi, mwanetu wenyewe, Salum Makamba. Yeye anatwambia tuLITUPE MTONI, tu. Ni kwenye Twiga Inflight Magazine, ndani ya Air Tanzania.
Muone kwanza!
UWARIDIII!

29/08/2023

KWA SABABU NAKUPENDA.

PENZI lilianzia shuleni; shuleni kabisa, tena Sekondari. Walijikuta wanazama ndani yake na kujiapiza kuwa, "Wakulitenganisha ni MUNGU" tena kwa kifo. Wakajidanganya na kuacha penzi lao lililomea k**a magugumaji nyikani lifike machoni mwa walimu. Likawa tatizo.

Daniel Lungwa, anajikuta anaingia matatani baada ya kujihusisha kimapenzi na mtoto wa mmiliki wa shule anayosoma; Josephine Malinzi.

Baba wa Jose anaharibu penzi lao na nusura ayaondoe maisha ya Dan, ni kudra za MUNGU ndizo zinamweka hai yule kijana. Anajiapiza hatoingia penzini tena.

Miaka minne ikatosha kuvunja kiapo chake. Maisha yakamwingiza kwa mara nyingine kwenye mapenzi. Lakini ni afadhali angeingia penzini na mwanamke mwingine, ingekuwa afadhali kubwa. Haikuwa hivyo bwana mdogo akarudisha majeshi kwa yuleyule ambaye ilibaki kidogo ampeleke kwenye nyumba ya milele. Akarudiana na Josephine ambaye kwa muda huo alikuwa msomi wa chuo kikuu huku yeye akiwa dereva bajaji.

Jambo ambalo alilijua wazi, ni kuwa Josephine ana mpenzi mwingine mwenye nguvu kifedha na asiyependa masikhara kwenye mali zake, ikiwemo penzi la Jose. Dan alifahamu fika lakini hakutaka kurudi nyuma. Akala na kusasambua mali za wakubwa. Likawa kosa lingine. Kosa ambalo linagharimu tena maisha yake.

KWA SABABU NAKUPENDA, riwaya inayoangazia suala zima la mapenzi na athari zake katika jamii.

Sasa riwaya hii inapatikana kwa Shilingi 12,000/- za Kitanzania sehemu zifuatazo:-

-Kona ya Riwaya, Kinondoni kwa simu namba 0655428085

-Na popote pale unapotaka kikufikie, piga, tuma ujumbe, whatsapp kwa 0627585638.

Hii si ya kukosa.
Karibu tufunue ukurasa kwa ukurasa.

Photos from Uwaridi Official's post 16/07/2023

KUTOKA KWA BINGWA WA TAHARUKI NCHINI.

Bingwa wa taharuki HUSSEIN TUWA ametuletea upya nakala za vitabu vyake vinne kwa mpigo, vikiwa vimechapwa upya kwa UBORA WA HALI YA JUU.

Kwa msioujua ubingwa wa mwamba huyu, ni kwamba yeye ndiye mwandishi pekee ambaye ameweza kuinyambua taharuki nje-ndani, nyuzi kwa nyuzi, huku akihakikisha unabaki naye sako kwa bako hadi mwisho wa kisa, kwenye usimuliaji wake.

Sasa k**a hujawahi kukutana na “Taharuki ya Mwendokasi,” basi sasa kaileta tena MKIMBIZI (ndiyo, ile ya Tigga-Mu, ile), kwa bei rafiki sana ya elfu 15 tu.

Na ikiwa hujapata kukutana na “Taharuki yenye Kasi ya Muziki wa Chacha,” basi katuletea tena WIMBO WA GAIDI, nayo kwa bei ile ile ya kirafiki ya shilingi elfu 15 tu.

Lakini ikiwa hukutaraji kusikia “Taharuki Roho Juu,” basi katuletea tena MDUNGUAJI, nayo bei yake ni k**a ya hivyo vingine tu.

Unaweza kusema kuwa umeshaona taharuki zote, kumbe ukawa hujawahi kukutana na “Taharuki Sisimuzi.” Basi huyu mwamba kaileta tena MTAFITI, ili akusisimue kwa ile ile elfu 15.

Inafikirisha eenh? (Basi huyu mwamba pia anayo “Taharuki Fikirishi,” hebu k**ata MISS TZ uone utakavyofikirika kitaharuki. Lakini hii bei yake ni elfu 25 kwa sababu inabeba vitabu viwili (2 in 1).

Bado una mashaka na ubingwa wa taharuki wa huyu bingwa?

Kupata nakala za vitabu hivi, hebu tembelea huku:

DAR ES SALAAM:
1) Duka la Kona ya Riwaya, Kinondoni Block 41 (0655 428085).

2) Posta Mpya round about "Kwa George," (0755 454152).

3) Elite Bookstore, Tangi Bovu (0767 740 363).

4) TPH Bookshop, Samora Avenue.

MIKOANI:

ARUSHA - BOOK POINT (0677 202 786); na BORA Bookshop ( 0784 499 844)

DODOMA — APE Bookshop, Shopper’s Plaza (0745199860); na BORA Bookshop (0622 105 628)

MOSHI — APE Bookshop (0755 239 911).

MWANZA - SETLIFE Bookshop (0786 390 201) na GAMMA Bookshop (0756 766 419)

Kwa maeneo mengine nje ya haya, au kwa maelezo zaidi, wasiliana nasi kupitia namba: 0655 428085 au 0784 122 598.

kutoka kwa

12/05/2023

TUNAENDELEA KUKIPAISHA KISWAHILI kupitia TWIGA InFlight Magazine, ndani ya AIR TANZANIA!
Safari hii ni kupitia kisa cha "NDOA YA SAA 24" kutoka kwa mwanadada mwingine kutoka UWARIDI, Agnes Mgonji!

UWARIDIIII!!!

30/04/2023

Salaam kutoka kwa akina dada wa UWARIDI.

25/04/2023

Kongole kwa Serikali kwa kufanikisha Tuzo za Uandishi Bunifu

SIKU ya Alhamisi, tarehe 13 Oktoba 2023 wakati dunia ikikumbuka miaka 101 tangu kuzaliwa kwa miongoni mwa viongozi wa Kiafrika mashuhuri, na Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere; tukio adhimu lilifanyika katika hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam, jiji ambalo kwa miaka mingi limeendelea kuwa kitovu cha uandishi bunifu. Hivyo, haikuwa bahati kwa mbaya tukio hilo kufanyika katika jiji hilo lenye utajiri wa historia na utamaduni wa Fasihi ya Kiswahili.

Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu.

Na si nasibu kwa Tuzo hizi adhimu katika Fasihi ya Kiswahili kuitwa Mwalimu Nyerere. Mwalimu Nyerere amekuwa na mchango mkubwa katika ukuzaji wa Fasihi ya Kiswahili. Sisi k**a Umoja wa Waandishi wa Riwaya wenye Dira (UWARIDI) tunaona fahari kwa hatua hii tuliyoitamani kwa miaka mingi.

Na hapa tunapenda kurejea tuliyoyasema kufuatia kuzinduliwa kwa Tuzo hizi hapo Agosti 12, 2022, ambapo tulisema, “Uwepo wa Tuzo za uandishi bunifu kwenye nchi ni jambo la msingi na muhimu sana kwenye kuthaminisha kiwango cha fasihi andishi ya nchi husika.”

Na k**a tulivyotarajia, waandishi waliitikia Tuzo hii na kushiriki katika kupambania. Kwa hakika, hii inapanua wigo wa uwanda wa Fasihi ya Kiswahili nchini mwetu. Tunazidi kusikia fahari kwamba, tukio hili ambalo Mgeni Rasmi wake alikuwa Rais mstaafu wa Msumbiji, Joaquim Chissano - miongoni wa Waafrika wanaozungumza vema lugha ya Kiswahili, linaiheshimisha vilivyo fasihi yetu.

Kwa dhati, tunaipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikisha hili. Na tunafurahi kuona kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolph Mkenda ametekeleza ahadi yake aliyopata kuitoa huko nyuma, ikiwamo wakati wa Tamasha la Fasihi la Elite Mjue Mtunzi, juu ya ujio wa Tuzo hizi. Vilevile, tunaipongeza Taasisi ya Elimu Tanzania kwa kusimamia na kuratibu shughuli nzima ya utolewaji wa Tuzo hizi; bila kuisahau K**ati ya Tuzo na jopo la majaji kwa kufanya kazi kwa weledi na juhudi katika kupitia mawasilisho ambayo hapana shaka yalikuwa lukuki, ili hatimaye kuwapata washindi.

Hakika ilikuwa ni furaha kubwa kuwaona waandishi nguli kutoka ndani na nje ya nchi, wakishiriki kutaja washindi, kugawa tuzo, na kusoma sehemu ya riwaya mbalimbali pale ukumbini - ambapo kutoka hapa nchini, Bi. Lilian Mbaga na mama Elieshi Lema waliwawakilisha waandishi wa ndani ya nchi kwa kusoma sehemu za riwaya zao.

UWARIDI, tunawapongeza washindi wote katika Riwaya na Ushairi na tunawaombea makubwa zaidi na tuzo nyingi zaidi.

Kwa kuwa hizi ni Tuzo za kwanza kabisa kufanywa na serikali yetu katika Fasihi ya Kiswahili, tunayo imani kubwa kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Taasisi ya Elimu pamoja na K**ati ya Tuzo wanayo mengi watakayokuwa wamejifunza, ambayo hapana shaka, watayatumia katika kuzidi kuziboresha Tuzo zijazo. Nasi UWARIDI tutaendelea kushiriki katika kutoa maoni juu ya uboreshaji na uhamasishaji kwa wanachama wetu na waandishi wengine kuendelea kuandika kwa juhudi na maarifa na kujifunga vibwebwe kushiriki kikamilifu katika Tuzo hizi zinazofaharisha Fasihi ya Kiswahili, lugha ambayo nguli wetu Sheikh Shaaban Robert ameisema kuwa tamu mithili ya t**i la mama.

Kwa kumalizia, sisi UWARIDI tunawatakia kila la kheri washindi wote kwenye safari yao ya uandishi bunifu huku tukiamini kuwa wametia chachu maridhawa kwa waandishi wengine wengi kwenye maandalizi ya Tuzo zijazo ili nao washiriki katika misimu ijayo.

UWARIDI(Njoo Tunukie)
Aprili 25, 2023.

Want your organization to be the top-listed Non Profit Organization in Dar es Salaam?
Click here to claim your Sponsored Listing.

Videos (show all)

Hongera LAURA!
Takribani watu milioni mia mbili Duniani tunazungumza Kiswahili—na kukifanya kuwa lugha ya nane kati ya lugha elfu sita ...
Waandishi wa Vitabu wanaomvutia Mzee Shafi Adam Shafi...
Mtangazaji wa Azam TV  na mdau mkubwa wa vitabu nchini, Bwana Moses Mohamed akisema mawili matatu kuhusu Mjue Mtunzi  (t...
ADA YA MJA KUNENA, MUUNGWANA NI VITENDO!Heri ya mwaka Mpya wa 2023 wadau wote wa fasihi andishi! Tukiwa tumeanza mwaka m...
Ahsante sana 2022. Mengi tumeyafanya katika utawala wako. Karibu 2023: ukawe mwaka wenye wingi wa heri kwetu, kwa waandi...
HAPPY NEW YEAR!
Hapa bingwa wa Taharuki akishiriki mjadala wa namna alivyojikuta akitamani kuwa mwandishi. Ni pale kwenye Maonesho ya 31...
TUKUTANE KWENYE TAMASHA LA 31 LA KIMATAIFA LA VITABU TANZANIA! Ni tarehe 11 mpaka 15 Oktoba, 2022 - Viwanja vya Posta, K...
Kuhusu simulizi ya KABRASHA LA RAIS... Mtunzi na Mwandishi WILBARD MAKENE alikuwa na haya ya kutusimulia...!!...
Mhe. Waziri Mkenda amewapongeza sana AzamTv, Elite Bookstore na Simulizi na Sauti (SnS) kwa ku-support harakati hizi za ...

Telephone

Website

Address


Ilala
Dar Es Salaam
Other Community Organizations in Dar es Salaam (show all)
AFYA BORA KWETU AFYA BORA KWETU
Mlimani City
Dar Es Salaam

PATA HUDUMA ZA KIAFYA, USHAULI NA ELIMU JUU YA CHANGAMOTO MBALI MBALI ZA KIAFYA, KWA KUTUMIA VIRUTUBISHO LISHE ASILIA VILIVYOZIBITISHWA KWA UBORA WA HALI YA JUU KUTOKA BFSUMA.

CPHEO Tanzania CPHEO Tanzania
Mkwinda Street 68
Dar Es Salaam, 105948

CPHEO ILIANZISHWA NA WATUMIA DAWA ZA KULEVYA, NA SHUGHULI ZETU NI ELIMU NA HUDUMA KWA WATUMIA DAWA Z

Business Opportunity Business Opportunity
Mikochen A
Dar Es Salaam, DARESSALAAM

*CROWD1*���� What is crowd1?� 》Crowd1 is a network company or a club for networkers that is supporting online gaming and gam

Intercession Gathering Intercession Gathering
Dar Es Salaam

WE INTERCEDE WE READ THE WORD OF GOD WE MAKE DISCIPLES

Nguyekolism under Nguyekolist Nguyekolism under Nguyekolist
Masanga A At Gungu The Holy Land
Dar Es Salaam, 19

Don't be quite when joining in this page

Afya Muhimu Kwanza Afya Muhimu Kwanza
Dar Es Salaam

welcome

Jamii ya Freemasonry Jamii ya Freemasonry
Posta
Dar Es Salaam

Chama cha Freemason ndilo jawabu la ndoto zako,Tangu ukiwa mdogo sasa mtu mzima hujafikia ndoto zako ishi ukijua muhimu kutimiza ni sasa ukiwa katika familia hii,Mali bila kumwaga ...

Jukwaa La Wanazuoni Maswa - Juwama Jukwaa La Wanazuoni Maswa - Juwama
Dar Es Salaam

Ni jukwaa la kijamii lenye malengo ya ya kuelimisha , kuelekeza na KUSAIDIA jamii ya maswa na Tanzani

Elias john mhagama Elias john mhagama
Dar Es Salaam

Tunakodisha vifaa vya mapambo na kupamba sherehe yako kwa ubora stahiki kwa maelekezo na picha za mapambo follow@mkdecor instagram au @muchuboy

United president community_upc United president community_upc
Dar Es Salaam

Join Africa with one president by prezdar GoodLife superstar

CHAMA HURU Freemasons CHAMA HURU Freemasons
POSTA
Dar Es Salaam

JIUNGE BURE NA FREEMASON ILLUMINATE AU FIKA OFISI KWETU

Lambert foundation Lambert foundation
Dar Es Salaam

Vision A community free disease and poverty. Mission Support vulnerable Communities in poverty red